Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linapenda kutoa taarifa kwa umma kwamba matokeo ya uchaguzi awamu ya kwanza kwa waombaji wa programu za afya mkupuo wa Septemba 2022/2023 yametoka rasmi leo tarehe 15 Agosti, 2022.
Baraza lilipokea jumla ya maombi 31,158 (wanawake 15,711 (50.4%) na wanaume 15,447 (49.6%)) ambapo waombaji 28,316 (91%) wana sifa za kujiunga na program mbalimbali za afya. Kati ya waombaji hao wenye sifa, wanawake ni 14,229 (50.2%) na wanaume 14,087 (49.8%).
Aidha, jumla ya waombaji 20,407 (72%) ya wenye sifa, wanawake 10,426 (51%) na wanaume 9,981 (49%) wamechaguliwa kujiunga na programu mbalimbali za Afya zinazotolewa na Vyuo 208 katika awamu hii ya kwanza. Waombaji 7,909 (28%) wanawake 3,803 (48%) na wanaume 4,106 (52%) walio na sifa hawakuchaguliwa katika machaguo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwa pamoja na ushindani, uwezo mdogo wa vyuo walivyoomba kama inavyoelezwa katika wasifu (profile) wa kurasa zao za maombi.
Waombaji wote wanaweza kuangalia majibu yao kupitia tovuti ya baraza (www.nacte.go.tz) kwa kupitia kiunganishi bonyeza hapa kwa ajiliya kupata taarifa zaidi. Kwa wale waliofanikiwa kuchaguliwa, wanashauriwa kupakua fomu ya kujiunga na kuwasiliana na chuo moja kwa moja kwa ajili yakuthibitisha kukubali nafasi hiyo. Baraza linawaelekeza waombaji wote ambao hawapo tayari kujiunga na vyuo kufanya mawasiliano na vyuo husika kwa maelekezo zaidi. Waombaji wote ambao hawakuchaguliwa wanatakiwa kufuata maelekezo yaliyopo kwenye kurasa zao za maombi (profile zao) kwa kujaza machaguo mapya.
Aidha, Baraza linapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa dirisha la awamu ya pili limefunguliwa leo tarehe 15/08/2022 haditarehe 30/08/2022 na matokeo ya uchaguzi yatatolewa tarehe 6/9/2022. Pia mfumo utafunguliwa tena kwa ajili ya kutuma maombi awamu ya tatu tarehe 8/9/2022 hadi tarehe 23/9/2022 na majibu ya uhakiki yatatoka tarehe 30/09/2022 ili wanafunzi waweze kuripoti chuoni kuanzia tarehe 3/10/2022 hadi tarehe 18/10/2022.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA MAFUNZO YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET)
15/08/2022